Jumapili 2 Novemba 2025 - 23:41
Jamii ya Leo Inayahitajia Sulhu Zaidi Kuliko wlKakati Mwingine Wowote

Hawza/ Mtukufu Ayatullah Nuri Hamadani amebainisha kuwa: leo jamii ya Kiislamu inayahitaji sulhu kwa kiwango cha juu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwani mashetani na maadui hutafuta njia ya kupenya kupitia migawanyiko na husuda za ndani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, ujumbe kamili wa Ayatullah Nuri Hamadani alioutoa katika mkutano wa kamati ya subira (Amani; Msamaha; Kuridhika) ni kama ifuatavyo:

بسْمِ اللَّهِ الرَّحْمنِ الرَّحیمِ

الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِینَ وَ الصَّلَاةُ وَ السَّلَامُ عَلَی سَیِّدِنا وَ نَبِیِّنَا أَبِی ‌الْقَاسِمِ المصطفی مُحَمَّد وَ عَلَی أهلِ بَیتِهِ الطَّیِّبِینَ الطَّاهِرِینَ سیَّما بَقیَّهَ اللهِ فِی الأرَضینَ و لعنة الله علی أعدائهم أجمعین إلی یوم الدین.

Uislamu ni dini ya rehema na huruma, maadili na uadilifu; dini iliyounganisha uadilifu na ihsani, na hukumu na sulhu na msamaha. Utamaduni wa amani, msamaha, na juhudi za wapatanishi wenye nia njema katika kuondoa migogoro na chuki, na kuimarisha mahusiano ya kijamii, ni miongoni mwa mafundisho bora kabisa ya Qur’ani Tukufu na Ahlul-Bayt wa Isma na watoharifu (a.s.), na ni alama ya imani na taqwa.

Miongoni mwa wasia wa milele wa Bwana wetu, Amirul-Mu’minin Ali bin Abi Talib (a.s.), kwa wanawe watukufu, Imam Hasan na Imam Husein (a.s.), wakati Ibn Muljim (laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) alipomjeruhi, ni hauu:

«أُوصِیکُمَا وَجَمِیعَ وَلَدِی وَأَهْلِی وَمَنْ بَلَغَهُ کِتَابِی بِتَقْوَی اللَّهِ وَنَظْمِ أَمْرِکُمْ ... وَصَلَاحِ ذَاتِ بَیْنِکُمْ، فَإِنِّی سَمِعْتُ جَدَّکُمَا صَلَّی اللهُ عَلَیْهِ وَآلِهِ یَقُولُ: صَلَاحُ ذَاتِ الْبَیْنِ أَفْضَلُ مِنْ عَامَّةِ الصَّلَاةِ وَالصِّیَامِ.»

“Ninakuusieni ninyi wawili, na watoto wangu wote, na watu wa nyumbani kwangu, na kila atakayefikiwa na barua yangu, muwe mumche Mwenyezi Mungu, muwe na nidhamu katika mambo yenu ... na Iswlah Dhat al-Bayn (kupatanisha baina yenu), kwani nimemsikia babu yenu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akisema: Iswlah Dhat al-Bayn ni bora kuliko Swala na Saumu nyingi.”

Imam Aly (a.s.) katika wosia huo ameeleza kuwa upatanisho baina ya watu ni bora kuliko ibada nyingi za Swala na Saumu, kwa sababu kuleta ukaribu wa mioyo, kuondoa chuki na kupatanisha baina ya waumini kunaleta umoja, maelewano na mapenzi katika jamii. Kuuunganisha mioyo ya waliofarakana au kupatanisha koo mbili zilizo na chuki au kutokuelewana, kunaleta thawabu kubwa kuliko ibada za sunna.

Leo pia, jamii yetu ya Kiislamu inayahitaji zaidi hili kuliko wakati mwingine wowote, kwani mashetani na maadui hutafuta njia ya kupenya kupitia migawanyiko na husuda za ndani. “Iswlah Dhat al-Bayn” ni kuziba mlango wa kupenya adui kupitia umoja na uaminifu wa pande zote.

Jamii ambayo roho ya msamaha na kuvumiliana imo hai, itakuwa salama kutokana na migogoro na uhasama, na msingi wa familia na uaminifu wa kijamii utapata uimara ndani yake.

Kwa mujibu wa fiqhi ya Ahlul-Bayt (a.s.), ni sunna yenye kusisitizwa kwa kadhi kuwataka waleta kesi wapatanishwe kabla ya kutoa hukumu, jambo ambalo ni dalili ya uadilifu na rehema. Kama alivyoandika faqihi mkubwa wa Kishia, mwandishi wa Jawahir al-Kalam, Shaykh Muhammad Hasan Najafi (ra):

«یُستحبّ ترغیبهما فی الصلح الذی هو خیر، ولا ینافی ذلک فوریة القضاء عرفاً»

“Inapendekezwa kuwahimiza wawili hao wapate suluhu ambayo ni bora, na hilo halipingani na dharura ya kutoa hukumu kwa wakati.”
(Jawahir al-Kalam, Juzuu ya 40, uk. 145).

Kwa msingi huo, juhudi za kuondoa chuki na kutatua migogoro kwa njia zisizo za kisheria (nje ya mahakama) ni bora kuliko kuipeleka kesi mahakamani.

Kwa hivyo, juhudi zenu zenye thamani katika Kamati ya Subira (Amani, Msamaha na Kuridhika) katika nyanja za upatanisho, uvumilivu na kutafuta suluhu za kimaadili na kijamii, ni miongoni mwa matendo mema kabisa. Amani na msamaha wakati wa kuwa na uwezo si dalili ya udhaifu, bali ni ishara ya nguvu ya kiroho, imani, na uhusiano kati ya fiqhi, maadili na uadilifu wa kijamii.

Wajibu wenu katika Kamati ya Subira si tu kupunguza idadi ya kesi, bali ni kufufua roho ya imani, kujenga upya uaminifu wa kijamii, kuimarisha msingi wa familia, kuimarisha undugu, maelewano na uhusiano wa kimaadili ndani ya jamii.

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameahidi:

«فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَی اللَّهِ»

“Basi anayesamehe na akafanya suluhu, ujira wake uko kwa Mwenyezi Mungu.”
(Surat Ash-Shura, aya 40)

Na pia amesema:

«وَالْکَاظِمِینَ الْغَیْظَ وَالْعَافِینَ عَنِ النَّاسِ وَاللَّهُ یُحِبُّ الْمُحْسِنِینَ»

“Na wanadhiti ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”
(Surat Aal-Imran, aya 134)

Mimi, pamoja na kutoa shukrani na pongezi kutokana na juhudi za dhati za viongozi na wahusika wa Kamati ya Subira (Amani; Msamaha; Kuridhika), nasisitiza mambo yafuatayo:

1. Sulhu na msamaha vinapaswa kujengwa juu ya imani, taqwa, uadilifu, ihsani, mtazamo wa mbali na kuridhika moyo; upatanisho unaotokana na shinikizo au dharura hautadumu.

2. Ushiriki wa wanazuoni, wasomi wa kitamaduni, wazee wa heshima, wakuu wa koo na makabila, na watu wanaoaminika katika jamii katika upatanisho ni tendo linalopendeza mbele ya Mwenyezi Mungu na lina thawabu kubwa ya kiroho.

3. Taasisi zote, mashirika ya serikali na ya kiraia, pamoja na watu binafsi na wa kisheria, wanapaswa kuisaidia Kamati ya Subira katika jukumu lake la kidini na kijamii.

4. Msamaha na kuvumiliana ni kielelezo cha nguvu ya maadili na ni muamala wa kiakhera; kamwe havipaswi kuchukuliwa kuwa ni dalili ya udhaifu. Shikeni kwa uthabiti uamuzi wa kusamehe na kupatanisha, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwa kutawassali na Ahlul-Bayt (a.s.); na kamwe msiwe chini ya ushawishi wa shetani au watu wanaozuia sulhu na upatanisho. Bila shaka, baraka za amani na msamaha mtazihisi zaidi katika maisha yenu kuliko matokeo ya kulipiza kisasi.

5. Wahusika wa Kamati ya Subira wanapaswa, kama taasisi inayotekeleza amani na kuimarisha maadili ya kijamii endelevu, kuzidisha kila siku uhusiano wa sheria na maadili, na wa hukumu na rehema.

Mwisho, namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ajaalie rehema maalumu za Baqiyyatullah al-A‘zam, Sahib al-Amr wa az-Zamaan (a.f.) kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa tukufu la Iran, na watendaji waaminifu katika sekta hii; na atujalie sote tawfiq wa kuimarisha maelewano, umoja wa kijamii, kuondoa kinyongo, kuimarisha familia, na kustawisha roho ya msamaha na mapenzi; ili jamii yetu ya Kiislamu, kwa baraka ya imani na mshikamano, iwe mfano wa Aya tukufu hii:

«وَمَن یَفْعَلْ ذَلِکَ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّهِ فَسَوْفَ نُؤْتِیهِ أَجْرًا عَظِیمًا»

“Na mwenye kufanya hivyo kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, basi tutampa ujira mkubwa.”
(Surat an-Nisā’, Aya ya 114)

Wassalamu ‘alaykum warahmatullahi wabarakatuh.

Husayn Nuri Hamadani

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha